HabariNews

Ubunifu biashara! Vijana watumia Makumbi ya Mnazi Kutengeneza Mazulia kaunti ya Kwale

Kama njia ya kuwaondoa vijana maskani na kuwatoa katika utumizi wa mihadarati kikundi kimoja cha vijana kaunti ya Kwale kimejitokeza kuwawahusisha vijana wenzao katika shughuli ya kutengeza mazulia.

 Kikundi hicho cha vijana cha KOREDO kimejitokeza kuwapa mafunzo ya kutengeneza mazuilia kutokana na makumbi ya mnazi eneo hilo ili kujibunia nafasi za ajira na kujiendeleza.

Kelvin Omondi kijana kutoka Kikundi hicho anasema kutokana na kutokuwa na ajira miongoni mwa vijana waliamua kuajiri vijana wa maskani na kina mama kuwasaidia katika kukusanya makumbi ya mnazi ambayo husagwa na kutumika kutengeneza mazulia ambayo yanawafaidi kwa kifedha za kujikimu.

Tumefanikiwa kuhamasisha vijana na kujipatia ajira na kipato, sasa hivi hawakai maskani kubweteka bure na kula mogokaa (miraa) wanajishughulisha na kuwajibika, Kwa njia hii tumewapa mama wajane na vijana ajira kutusaidia kukusanya makumbi na pia wao wanapata kujikimu kiajira.” Alisema.

Omondi alisema mbali na kuwa wanabuni nafasi za ajira aidha njia mojawapo ya kudumisha usafi wa mazingira na kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.

“Tunatumia malighafi ambayo ni Makumbi kutoka kwa wakulima wa mashamba ya minazi, haya makumbi tunayasaga na tunatengeneza nyuzi kutokana na Makumbi hayo na kutengeza mazulia ya kuweka mlangoni (doormats)…Haya makumbi kina mama wakiyapikia ule moshi inawaathiri macho na mazingira.” Alisema Pia alisema wanatumia unga wa makumbi kuoteshea miche katika mashamba.

Shirika hilo lililo na miaka mitatu tangu kubuniwa kwake hata hivyo limeeleza kuwa na changamoto ya kuendeleza mradi huo kutokana na gharama ya juu ya vifaa vya kusagia makumbi pamoja na leseni kutoka kwa Halmashauri ya mazingira NEMA na ile ya kaunti kuendesha biashara na mtambo huo.

Wametaka kaunti na idara nyinginezo hasa NEMA kuwapunguzia ada za biashara na usafirishaji wa bidhaa zao ili kuwapa vijana nafasi za kipato.

BY BINTIKHAMIS KADIDE