Habari

Wakaazi wa kijiji cha Hawewanje huko Chakama eneo bunge la Magarini Kaunti ya Kilifi wamefanya maandamano ya amani wakilalamikia kunyakuliwa kwa ardhi wanayoishi.

Wakiongozwa na Kazungu Nyale Baraka na Eunice Katana Bao,wakaazi hao wanamnyoshea kidole cha lawama Chifu wa eneo hilo Macdonald Ngowa wakidai anashirikiana na mabwenyenye kunyakua ardhi ya ekari zaidi ya elfu moja.

 

Wakaazi hao sasa wanaitaka Serikali kuwapimia ardhi hiyo na ihakikishe wanapata hati miliki zao kwani kwa muda mrefu wameishi kama maskwota.

Mzee wa Kijiji wa Hawewanje Mwambegu Kahindi anadai Bwenyenye mmoja aliwahadaa wakaazi kwamba kuna mradi unataka kutekelezwa huku akishirikiana na maafisa kunyakua kipande hicho cha ardhi.

 

Aidha Mzee huyo amemkashifu vikali Chifu wa eneo hilo akisema amekuwa mstari wa mbele kuuza mashamba ya eneo hilo, hivi majuzi zaidi ya ekari 400 kati ya elfu moja zilizoko eneo hilo zikiuzwa kwa njia tatanishi.

 

Hata hivyo juhudi zetu za kumpata Chifu Mwaringa Ngowa ziliambulia patupu kwani chifu huyo hakupokea simu zetu.