Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i amelipa shirika la UNHCR makataa ya siku 14 kuja na ramani ya kufungwa kwa kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma.
Matiang’i alisema hakuna nafasi ya mazungumzo zaidi.
Ameyasema hayo alipokutana na ujumbe kutoka kwa mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya Fadhilaa Addala siku ya Jumanne ofisini mwake.
Matiang’i ambaye alikuwa ameandamana na Katibu mwandamizi katika afisi yake Hussein Dhado na Katibu wa kudumu Karanja Kibicho alitaja vitisho vya ugaidi vinavyopangwa kutoka kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma.
Alisema pia Kenya na Somalia hazina uhusiano wa kidiplomasia kuendelea kuwa mwenyeji wa wakimbizi wa nchi hiyo.
Serikali pia imepanga mkutano mwingine na wanadiplomasia kutoka Rwanda, Burundi, Uganda na Sudan Kusini siku ya Ijumaa ili kurekebisha urejeshwaji wa raia wao kutoka kambi hizo.