Habari

Jaji Koome asema, kuwa mwanamke sio kizuizi cha kuwania wadhfa wa jaji mkuu…….

Shughuli ya kumuhoji jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome kwa wadhfa wa jaji mkuu inaendela kwa sasa ambapo amepata fursa ya kujieleza mbele ya jopo la makamishna wa tume ya huduma za mahakama JSC.

Akijieleza Koome anasema amepata fursa ya kuhdumu katika sekta ya uanasheria kwa miaka 15 katika Nyanja mbali mbali kabla ya kuwa jaji.

Amesema akiwa mwenyekiti wa chama cha mahakimu yuko kwenye nafasi nzuri ya kushughulikia masuala mbali mbali katika idara ya mahakama akisema anaelewa vizuri utendakazi kwenye idara hiyo.

Amesema suala la kuwa mwanamke sio kizuizi cha kuwania wadhfa wa jaji mkuu, ambao awali wadhfa huo ulishikiliwa na wanaume akisisitiza kwamba masuala ya uongozi hayajali jinsi.

Alipotakiwa kueleza ni hatua gani atachukuwa iwapo kutakuwa na ukosefu wa maelewano miongoni mwa majaji wa mahakama ya juu, ameeleza kwamba huenda akalazimika kuitisha kikao maalum cha majaji hao ili kupata muafaka na kushughulikia matatizo yalipo.

Kuhusiana na ufafanuzi wake kuhusu masuala ya haki ya kumiliki mali katika ndoa ikizingatiwa uwepo wa mizozo mingi, amesema mtu hana haki ya kupigania mali ambayo mwenzake aliipata kabla ya kuingia ndani ya ndoa.

Vikao vya kumrithi Maraga vinaongozwa na makamishna tisa wa tume ya JSC, ambao ni kaimu jaji mkuu Philomena Mwilu, naibu mwenyekiti wa JSC Olive Mugenda, Jaji Mohammed Warsame, mwanasheria mkuu Kihara Kariuki, miongoni mwa wanachama wengine.