HabariNews

Kizaazaa chashuhudiwa katika mazishi ya Zainab Chidzuga…..

Kizaa kimeibuka katika mazishi ya aliyekuwa mwakilishi wa kike wa kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga baada ya mwenyekiti wa chama cha Wiper Chirau Mwakwere kumkataza katibu mkuu wa wizara ya kilimo proffesa Hamadi Boga kuwahutubia waombolezaji.

Hali hiyo ilisababisha waombolezaji hao kumzomea vikali Mwakwere wakitaka Boga kupewa ruhusa ya kuzungumza.

Kwa mujibu wa Makwere , Boga pamoja na viongozi wengine walivuruga ratiba ya mazishi ya marehemu bila ya kuhusisha familia yake.

Hatua ya Mwakwere kumzuia Boga kuzungumza imetajwa kuchochewa kisiasa ikizingatiwa kwamba viongozi hao wote wawili wanamezea mate wadhfa wa ugavana katika uchaguzi mkuu ujao.

Boga alikuwa ametumwa kusoma risala za rambi rambi za rais Uhuru Kenyatta.

Mwakwere pia amenyima fursa katibu katika wizara ya utalii Safina Kwekwe kuusoma ujumbe huo wa rais, ambapo Boga alikuwa amemkabidhi kuusoma kwa niaba yake.

Licha ya mtoto wa Marehemu Mariam Chidzuga kumrai Makwere juhudi zake hazikufua dafu hatua iliyosababisha baadhi ya waombolezaji na viongozi kuondoka.

Hali hii ilisababisha wabunge Khatib Mwashetani wa LUNGA Lunga na Benjamin Tayari wa Kinango kuondoka kwenye hafla hiyo.

Chidzuga alifariki dunia hapo jana katika hospitali ya Reliance iliyoko Nairobi ambako alikuwa anatibiwa ugonjwa wa covid 19.

Marehemu amezikwa adhuhuri ya leo nyumbani kwake huko Golini Matuga kaunti ya Kwale.

By Kwale Correspondent