HabariMazingira

Hali ya ukame inaendelea kuwa mbaya humu nchini…….

Hali ya ukame inaendelea kuwa mbaya zaidi humu nchini huku kaunti nne zikitajwa kuendelea kuathirika zaidi wakati wakaazi wakikumbwa na baa la njaa.

Kwa mujibu wa wizara ya ugatuzi nchini, familia kadhaa zinakumbwa na uhaba wa chakula kutokana na ukame.

Waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa ametaja serikali za kaunti ya Wajir, Marsabir, Isiolo na Garissa kuwa zilizoathiriwa na tayari zimeorodheshwa kuwa zitafanywa kipau mbele katika utoaji wa chakula cha msaada.

Wamalwa amesema kamati maalum imebuniwa kusaidia katika kutoa msaada kwa familia zilizoathiriwa.

Akizungumza huko Naivasha Wamalwa pia ametoa hundi ya shilingi milioni 575 kwa benki ya equity ili kuzisaidia familia zinazokumbwa na baa la njaa.

Wizara hiyo imesema kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa huenda ikaongezeka hadi na kufikia milioni mbili katika miezi ijayo, iwapo mvua haitaendelea kunyesha.

Haya yanajiri huku serikali ikipuuza taarifa kwamba kuna watu wamefariki dunia kutokana na makali ya njaa.

Serikali badala yake inasema kwamba wanaofariki ni wale ambao walikuwa wameambukizwa virusi vya corona katika kaunti ambazo zimekuwa zikishuhudia ukame.

 

By news team