Rais Uhuru Kenyatta amedokeza kwamba amri ya kutotoka nje nyakati za usiku kuanzia saa nne hadi saa kumi alfajiri maarufu Curfew ikaondolewa hivi karibuni.
Akihutubia wakazi katika eneo la Karatina alipokuwa akielekea Kirinyaga ambako maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ya mwaka huu yatafanyika, Rais Kenyatta ameahidi kwamba marufuku hayo yataondolewa ila hakutaja siku muafaka.
Kiongozi huyo wa taifa alikuwa akijibu wito wa wakaazi wa eneo hilo ambao walimuomba aondoe amri hiyo ambayo imedumu kwa takriban miaka miwili sasa tangu kutangazwa.
Wakati huo huo, Uhuru amewaonya wakaazi hao kuhusu Viongozi wanaowahadaa kwa kuwapa fedha kila mara wanapozuru eneo hilo.
Rais aidha amewahimiza wakaazi kuendelea kufuata kanuni kutoka kwa Wizara ya Afya, ili kuhakikisha wako salama kutokana na janga ambalo limeuumiza ulimwengu, kuua mamilioni, na virusi ambavyo vilidhoofisha uchumi wa nchi.
BY NEWS DESK