HabariNewsSiasa

Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula ameitisha mkutano wa Baraza la Kitaifa la Chama.

Hatimaye Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula ameitisha mkutano wa Baraza la Kitaifa la Chama ili kujadili masuala mbali mbali yanayokikumba Chama hicho.

Kulingana na taarifa Kiongozi huyo ametangaza mkutano huo kufanyika tarehe 4 Mwezi Novemba mwaka huu katika Ukumbi wa Bomas Jijini Nairobi.

Mkutano huo unajiri kufuatia mashinikizo ya Mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu ya kuandaa mkutano huo Novemba 6 katika Uwanja wa Kasarani.

Itakumbukwa kwamba wawili hao wamekuwa katika mgogoro kwa muda sasa, Eseli akidai kwamba Wetangula hafai kukiongoza Chama hicho kwa kuwa yuko mamlakani kinyume na sheria za Chama.

Eseli aliibua hali ambapo Wetangula hajawahi kuitisha mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la Chama kujadili masuala kadhaa Chamani vile vile kuwachagua viongozi wengine.

Mrengo wa Wetangula unasisitiza kwamba ndiye Kinara wa Ford Kenya na kupuuza madai ya Eseli.

BY NEWS DESK