HabariKimataifaNews

ZAMBIA YAADHIMISHA MIAKA 57 YA UHURU.

Zambia Jumapili ilifanya sherehe ya maadhimisho ya miaka 57 tangu ijipatie uhuru wake kutoka kwa Waingereza huku shamrashamra mbalimbali zikifanyika katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Rais Hakainde Hichilema aliongoza sherehe za kilele zilizofanyika Lusaka, mji mkuu wa nchi hiyo, iliyoanza kwa kuweka mashada ya maua kwenye sanamu ya Uhuru ili kuheshimu watu waliofariki wakati wakipigania uhuru wa nchi hiyo, kisha kuoneshwa mazoezi ya kijeshi ya vikosi vya ulinzi, na baadaye kwenda mahali wanapozikwa marais wa zamani wa nchi hiyo, ambapo rais Hakainde aliwaongoza viongozi wengine kuweka mashada ya maua.

Rais wa Zambia pia aliwatunuku watu kutoka sekta mbalimbali kwa mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Katika hotuba yake, rais wa Zambia alitoa wito kwa wananchi kuondoa tofauti zao na kuungana kwa manufaa ya nchi. Pia aliwataka wananchi kuonyesha uzalendo na kuendeleza umoja wa kitaifa. Ameongeza kuwa serikali ina nia ya kuendeleza nchi kupitia mageuzi ya kiuchumi, na kupitia mageuzi hayo, nchi hiyo itakuwa na uhakika wa chakula, kupunguza umaskini na kutoa ajira hasa kwa vijana.

BY NEWS DESK.