HabariKimataifaNews

SERIKALI YA MALI YASEMA IMEZIMA JARIBIO LA MAPINDUZI.

Serikali ya Mali inayoongozwa na kiongozi wa mapinguzi imetangaza kuwa vikosi vyake vya usalama vimezuia jaribio la mapinduzi ambalo imesema liliungwa mkono na nchi moja ya Magharibi ambayo haikutajwa.
Tangazo hilo ni msukosuko wa hivi punde zaidi kutokea Mali, ambako Kanali Assimi Goita aliongoza mapinduzi mara mbili katika mwaka wa 2020 na 2021 kabla ya kuwa rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga haikuitaja nchi ambayo inatuhumiwa kuunga mkono njama ya mapinduzi.
Hata hivyo, mahusiano na mtawala wake wa zamani Ufaransa yamedorora pakubwa chini ya uongozi wa Goita, hali iliyolilazimu jeshi la Ufaransa kuanza kuwaondoa askari wake ambao walikuwa nchini humo kwa miaka tisa wakipigana na wanamgambo wa itikadi kali.
Maiga amesema bila kutoa maelezo zaidi kuwa jaribio hilo la mapinduzi lilizimwa Jumatano wiki iliyopita akiongeza kuwa usalama umeimarishwa kwenye vituo vya ukaguzi kwenye barabara za kuondoka mji mkuu Bamako ili kuwasaka wahusika.

BY EDITORIAL DESK