HabariNews

Shirika la Association for the Physically Disabled of Kenya limeunga mkono utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu (CBC).

Shirika la Association for the Physically Disabled of Kenya limeunga mkono utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu (CBC) na serikali ya kitaifa.

Afisa wa shirika hilo katika eneo la Pwani Jemimah Kutata amesema kuwa mtaala huo unalenga kukuza talanta za wanafunzi katika shule za walemavu.

Akizungumza katika eneo la Lungalunga, Kutata amesema kwamba utekelezaji wa CBC utawafaa wanafunzi wenye changamoto ya ulemavu.

Kwa upande wake naibu kamishna wa Lungalunga Joseph Sawe amewataka wazazi katika eneo hilo kuwapeleka wanao wenye ulemavu shuleni.

Sawe ameahidi kushirikiana na shirika hilo ili kuhakikisha kwamba wazazi hawafichi wanao nyumbani.

Huku hayo yakijiri, changamoto imetolewa kwa serikali ya kitaifa kuwaajiri walimu wa kutosha katika shule za walemavu ili kufanikisha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu (CBC).

Kulingana na mkurugenzi wa shirika la Kids Care Ali Mwaziro, idadi kubwa ya shule hizo zinakumbwa na uhaba wa walimu katika eneo bunge la Lungalunga Kaunti ya Kwale.

Akizungumza katika hafla ya kuyakabidhi madarasa sita kwa serikali kuu yaliyojengwa na shirika hilo kwa takriban shilingi milioni 57, Mwaziro ameitaka serikali hiyo kuwapeleka walimu katika eneo hilo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa elimu katika eneo la Pwani Adan Roble ameahidi kuwa serikali inalenga kuwatuma walimu watatu katika kila shule.
Roble amewataka wazazi wenye watoto walemavu eneo hilo kuwapeleka shuleni badala ya kuwaficha nyumbani.

BY EDITORIAL TEAM