HabariNews

WAKULIMA ZAIDI YA 400 WAHUDHURIA MAFUNZO YA KUPANDA MITI KILIFI.

Wakulima zaidi ya 400 kutoka wadi ya Junju wamehudhuria mafunzo ya kuwahamasisha mbinu bora za ukulima wa mimea, ufugaji na upandaji wa miti, ili kukabiliana na athari za tabia nchi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa Junju Matendo CBO, Crispus Mwaganda, mafunzo hayo yanatokana na hali ngumu ambayo wanapitia wakulima kwa kukosa mavuno kutokana na kiangazi.

Anasema mbinu hizi zitaiwezesha kaunti hii kuwa na chakula cha kutosha licha ya kiangazi kikali kinachoshuhudiwa iwapo mbinu hizi zitazingatiwa.

Aidha amesema licha ya kukumbatia agizo la rais dkt. William Ruto la kuhakikisha kuwa watu wanapanda miti, wanakumbwa na changamoto ya kupata miche ya kutosha, huku wakiisihi serikali kuwasaidia.

Kwa upande wake Lenard Mambo ofisa wa kilimo wadi hii anasema hatua ya wakazi kukumbatia upandaji miti kutalisaidia taifa hili kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Diwani wa hapa Junju Said Juma Iddi ameeleza kuwa mikakati ya kuchimba mabwawa eneo hili inaendelea kupangwa ili kurahisisha shughuli za kilimo.

Hellen Mwarua na Lillian Ringa ni wanachama wa Junju Matendo CBO waliohudhuria mafunzo hayo.

BY ERICKSON KADZEHA.