Kamishena wa kaunti ya Kwale Gideon Oyagi amesema kuwa tayari serikali imetenga chakula cha msaada kwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa mwezi huu katika kaunti hiyo.
Akizungumza katika eneo la Diani, Oyagi amesema kwamba kamati ya kukabiliana na ukame kaunti hiyo itahakikisha chakula hicho kinawafikia walengwa.
Oyagi amesema kuwa chakula hicho kitatolewa kwa watahiniwa katika shule za kutwa na zile za msingi ili kuwakinga na makali ya njaa.
Wakati uo huo, kamishna huyo amedokeza kuwa maafisa wa usalama watapelekwa kushika doria katika vituo vya mtihani.
Oyagi amewataka wasimamizi wa mtihani huo kuhakikisha kwamba hakuna visa vyovyote vya udanganyifu vinatokea kaunti hiyo.
Jumla ya watahiniwa 24,494 wa KCPE, 10,485 wa KCSE na 25,913 wa mtaala mpya wa CBC (KPSEA) wanatarajiwa kufanya mtihani huo.
KPSEA – Kenya Primary School Education Assessment.
BY EDITORIAL TEAM