Watu zaidi ya elfu moja kutoka kwa jamii ya wavuvi wamepata suluhu ya
kudumu ya tatizo la maji ambalo limewakumba kwa muda mrefu, kufuatia
kuzinduliwa kwa kisima katika Bandari ya Old Ferry mjini Kilifi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliogharimu takriban
shilingi laki moja na nusu, diwani wa Sokoni Ray Mwaro Katana amesema
jamii ya wavuvi wamekuwa wakiendeleza shughuli zao katika mazingira
magumu kwa ukosefu wa maji safi.
Ameeleza kuwa anaendeleza mikakati ya kuhakikisha kuwa tatizo la maji
katika wadi ya Sokoni linapata suluhu ya kudumu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wavuvi katika bandari ya Old Ferry mjini
Kilifi Henry Chiko Mzungu anasema upatikanaji wa maji hayo utawafaidi
jamii hiyo ya wavuvi ambao ni zaidi ya elfu moja.
Rukia Pamba Juma mmoja wa wachuuzi wa samaki, anasema wavuvi wamekuwa
wakilazimika kutumia hela nyingi kununua maji ya kusafisha vifaa vyao
vya kazi hali anayobainisha kuwa imeifanya biashara yao kuwapa faida
ndogo.
BY ERICKSON KADZEHA