HabariNewsSiasa

GAVANA WA KILIFI ATIMIZA BAADHI YA AHADI ZAKE KATIKA SIKU 100 ZA KWANZA MAMLAKANI.

Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro amefanikiwa kutimiza baadhi ya ahadi alizotoa kwa wakazi wakati wa kampeni katika kipindi cha siku 100 za kwanza mamlakani haya ni kulingana na mtaalamu wa maswala ya Kilimo kaunti ya Kilifi.

Baadhi ya hoja zilizotajwa kupewa kipaumbele na gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro ni kuimarisha elimu, kuboresha afya na Kilimo miongoni mwa hoja nyingine.
 
Kwa mujibu wa mtaalamu wa maswala ya kilimo kaunti ya Kilifi Baha Nguma, anasema, moja ya hatua muhimu ambayo huenda ikaleta matumaini ya kukabiliana na baa la njaa kaunti ya Kilifi ni kuongezwa kwa fedha za kusimamia idara ya kilimo kutoka asilimia 7.5 hadi 10.
 
Anasema hatua iliyosalia ni mkaguzi wa hesabu za serikali kuipitisha bajeti hiyo baada ya bunge la kaunti ya Kilifi kufanyia marekebisho ugavi huo.Hata hivyo ametaja hatua za dharura zilizowekwa ili kuwasaidia wakaazi zaidi ya laki mbili ambao wanakumbwa na baa la njaa kaunti ya Kilifi, ambapo wakazi zaidi ya 50,000 walifanikiwa kupata usaidizi huo, huku takriban kilo 18,000 za chakula zikigawanywa katika shule za chekechea.

Kulingana na Mamlaka ya kukabiliana na ukame nchini, NDMA 2023, kaunti ya Kilifi ni miongoni mwa kaunti 13 zilizoorodheshwa kuathirika zaidi na baa la njaa.

BY ERICKSON KADZEHA