Mwanafunzi mmoja wa kike kutoka eneo bunge la Malindi, ameingilia biashara ya kusuka makuti ili kujipatia karo ya kujiunga na shule ya upili ya wasichana ya Kisoko.
Rabecca Salama kutoka kijiji cha Gahaleni, eneo bunge la Malindi aliyepata alama 329 kwenye mtihani wa kitaifa wa KCPE mnamo mwaka 2022, ameingilia kazi ya kusuka makuti ili kujipatia karo ya kujiunga na shule ya upili.
Salama ambaye alifanya mtihani wake wa kitaifa katika shule ya msingi ya Airport mjini Malindi, anasema aliamua kufanya uamuzi wa kusuka makuti kufuatia familia yake kukumbwa na changamoto ya umasikini.
Ameeleza kuwa licha ya kupata barua kuitwa kujiunga na shule ya upili ya wasichana ya Kisoko, iliyo kaunti ya Busia kizungumkuti cha karo, kimemkatisha matumaini ya kuendeleza masomo yake huku akiwaomba wahisani kujitokeza na kumsaidia kuendelea na masomo yake ya sekondari.
Kwa mujibu wa Lucy Mwangala, mama wa msichana huyo hali ngumu ya uchumi inayoikumba familia yake imechangia yeye kushindwa kumlipia mwanawe karo, huku akieleza kuwa juhudi zake za kutafuta ufadhili wa masomo ya mwanawe hazijafaulu.
Na sasa anaiomba serikali pamoja na wahisani kumsaidia mwanawe, ili aweze kujiunga na shule ya sekondari.
Ikumbukwe wanafunzi takriban milioni moja waliofanya mtihani wa kitaifa KCPE 2022 wanatarajiwa kujiunga na shule za upili mwaka huu.
BY ERICKSON KADZEHA.