HabariNews

Wapemba waahidiwa kutotengwa wanapotafuta huduma za serikali.

Maelfu ya watu wa jamii ya Wapemba wameahidiwa kutotengwa wanapotafuta huduma za serikali kufuatia shughuli ya kuwasajili kuwa raia wa Kenya kuzinduliwa rasmi jana Jumatano.

Kwenye uzinduzi huo, uliofanyika mjini Kilifi, katibu wa kudumu wa wizara ya uhamiaji na usajili wa watu Julius Bitok, alisema hakuna mwanajamii yeyote wa Kipemba, atakaye baguliwa wala kunyimwa huduma za serikali baada ya harakati hii ya kuwasajili kuwa raia wa Kenya kuanza rasmi.

Viongozi wa ukanda huu wa pwani wakiongozwa na mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mpango wa kuwasajili Wapemba zaidi ya elfu 7 kuwa raia wa Kenya unaidhinishwa, hii ikiwa moja wapo ya ahadi alizotoa mbunge huyu kwa jamii ya Wapemba wakati wa kampeni zake katika uchaguzi mkuu uliopita.

Hata hivyo aliongeza kuwa serikali ya kaunti hii ya Kilifi inafaa kuwajumuisha jamii ya Wapemba kwenye uongozi kwa kuwapa nyadhifa kwenye serikali hiyo.

Kwa upande wake gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro aliwahimiza jamii ya Wapemba kuharaikishiwa shughuli hiyo kwa ajili ya kujumuishwa kwenye mipango muhimu ya serikali kama misaada ya karo za shule na maendeleo ya kijamii.

Ikumbukwe tarehe 13 Mwezi wa tisa mwaka 2022 wakati wa hafla ya kuapishwa kwa rais wa tano wa taifa hili la Kenya, Rais William Ruto alileta matumaini mapya miongoni mwa maelfu ya watu wa jamii ya Wapemba humu nchini Kenya kwa kuahidi kutambuliwa kwa jamii hii wanaoishi kaunti za Kilifi, Mombasa na Kwale.

BY ERICKSON KADZEHA