HabariNewsTechnology

TEKNOLOJIA HUTUMIKA MIJINI KWA WINGI KULIKO MASHINANI.

Ulimwengu ukiadhimisha siku ya wanawake hii leo, imebainika kwamba
teknolojia inatumika sana na watu walio mijini ikilinganishwa na wale
walio mashinani.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ikiwa uvumbuzi na matumizi ya
teknolojia ili kuleta usawa wa jinsia, imebainika kuwa ni asilimia 37
pekee ya wanawake ulimwenguni wanaofanya kazi zinazohusiana na masuala
ya teknolojia huku asilimia 57 wakiwa na ufahamu wa matumizi ya
teknolojia ikilinganishwa na asilimia 62 ya wanaume wenye ufahamu huo.

Kwa mujibu wa mshirikishi wa masuala ya jinsia na maendeleo ya vijana
kaunti ya Kilifi Mwangome Shumaa, wanawake wengi katika sehemu za
mashinani hawana uelewa wowote wa teknolojia hivyo ametoa wito kwa
wanawake wenye taaluma za teknolojia kuwahamasisha wanawake wengine ili
kujikuza kibiashara kupitia mitandao.

Kwa upande wake afisa wa shirika la kijamii la KECOSCE Kibwana Hassan,
amesema kuna haja ya serikali ya kaunti kusambaza teknolojia kila eneo
hata mashinani hasa ngamiza yaani internet.

Anasema kukosekana kwa interneti na ufahamu wa teknolojia kumepelekea
wanawake wengi walio mashinani kukosa nafasi muhimu za kujiendeleza
kimaisha.

Baadhi ya wanawake na wasichana mjini Kilifi wamekuwa na haya ya kusema
kuhusu kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake ulimwenguni ambayo
yanafanyika kijijini Takaungu eneo bunge la Kilifi Kaskazini.

BY ERICKSON KADZEHA.