HabariNews

VIWANGO VYA ELIMU YA SEKONDARI MSINGI NI DUNI YASEMA KUPPET.

Viwango vya elimu ya sekondari msingi ni duni humu nchini kufuatia kushuhudiwa kwa uhaba wa walimu wa kufunza mtaala huo mpya, miundo msingi duni miongoni mwa changamoto nyingine imesema KUPPET.

Kaunti ya Kilifi ikiwa miongoni mwa maeneo yanashuhudia uhaba huo wa walimu, kufikia sasa kaunti hii inakadiriwa kuwa na takriban walimu elfu moja wanaofunza kwenye zaidi ya shule za sekondari msingi 553.

Kwa mujibu wa katibu mtendaji wa chama cha walimu wa sekondari na vyuo vya kati nchini KUPPET kaunti ya Kilifi Caleb Mogere, uhaba huo wa walimu umewalazimu walimu kufunza madarasa zaidi ya mawili ili shughuli za masomo ziendelee kama kawaida.

Amesema viwango vya elimu inayoendelea kutolewa ni duni kufuatia kukosekana kwa vifaa muhimu vya masomo kama vile kukosekana kwa maabara shuleni, madarasa machache, miongoni mwa mambo mengine.

Amesisitiza kuwa haki ya wanafunzi inakiukwa kwa kupewa elimu duni huku akiihmiza serikali kujizatiti ili kutatua changamoto hiyo katika mfumo huo wa elimu.

BY ERICKSON KADZEHA.