HabariNews

Sera duni za kutathmini masuala ya maji kaunti ya Kwale zimechangia ukosefu wa maji.

Wadau wa kutetea haki za kibinadam Kaunti ya Kwale wanasema Sera duni za kutathmini masuala ya maji kaunti ya Kwale zimechangia ukosefu wa maji ya kutosha licha ya kaunti hiyo kuaminika kuwa na vyanzo vikuu vya maji na chemichemi nyingi za maji safi.

Afisa wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Huria, Alex Nziwi amedokeza kuwa sera duni ambazo hazijatilia mkazo jinsi wakaazi wa Kwale wanaweza kunufaika na raslimali waliyonayo zinapelekea wakaazi kutaabika na bidhaa hiyo muhimu jambo alililolitaja kuhujumu haki ya wananchi.

Nziwi amesema  kuwa licha ya Kwale kuwa na chemichemi na vyanzo vikuu vya maji ikiwemo Marere, wananchi hawanufaiki na maji.

Afisaa huyo wa Huria amelitaka bunge la kaunti ya Kwale kuja na sheria itakayohakikisha maji kaunti ya Kwale yanawafaidi wakaazi wenyewe badala ya kuuzwa kaunti jirani ya Mombasa.

Ameongeza tayari wanakusanyana sahihi kuhakikisha wanaskuma swala hilo la raslimali ya maji bungeni.

BY EDITORIAL DESK