HabariNews

MRADI WA MAJI WA BAMBA- SHIRANGO KAUNTI YA KILIFI WAZINDULIWA RASMI.

Waziri wa maji nchini Alice Wahome  amezindua rasmi mradi wa maji
Bamba-Shirango katika kijiji cha Rima Pera eneo Bunge la Ganze, mradi
unaotarajiwa kuwa utamaliza tatizo la uhaba wa maji eneo hilo.

Mradi huo wa maji wa Bamba-Shirango utahudumia eneo la takriban Kilomita
73 mraba huku ukitarajiwa kuwanufaisha watu zaidi ya 11,000.

Kulingana na waziri wa maji nchini Alice Wahome mradi huo ni moja wapo
ya mbiu za kutafuta suluhu ya tatizo la uhaba wa maji ambao umekuwa
ukishuhudiwa kwa muda mrefu eneo hili huku akiahidi ushirikiano kati ya
serikali ya kitaifa na ile ya kaunti ya Kilifi katika kuendeleza miradi
ya maji.

Gavana wa Kilifi, Gideon Mungaro amesistiza kwa mara nyingine kuwa
watashirikiana na serikali ya kitaifa kuhakikisha wanapata suluhu ya
tatizo la maji huku akieleza kwamba kaunti ya Kilifi itajenga matangi
yatakayohifadhi takriban lita 5,000,000 za maji ili wakaazi wapate maji
ya kukidhi mahitaji yao kila siku.

Waziri wa maji kaunti ya Kilifi Omar Said Omar amesema tatizo kuu
linalosababisha uhaba wa maji safi kaunti ya kilifi ni gharama ya juu ya
umeme unaotumika kusambaza maji akimtaka waziri Wahome kuliangazia zaidi
swala hilo ili wakazi waweze kupata maji safi.

BY ERICKSON KADZEHA.