Hali ya uchumi kudorora ikiendelea kushuhudiwa humu nchini, wadadisi wa masuala ya uchumi wanasema taifa linazidi kuelekea pabaya kufuatia changamoto hiyo, huku wakiwataka viongozi kutafuta suluhu ya haraka badaya ya kulumbana hadharani.
Profesa Halimu Shauri mhadhiri wa sayansi na maendeleo ya jamii katika chuo kikuu cha Pwani anasema uchumi ndio tegemeo na nguzo zote za maisha ya binadamu, akionya kuwa pasi swala hili kushughulikiwa kwa umakini mkubwa na kitaalamu huenda likasababisha athari kubwa katika taifa hili.
Swala la kuzorota kwa uchumi limeshuhudiwa enzi za hayati marais wastaafu Daniel Arap Moi, pamoja na Mwai Kibaki, waliolazimika kuunda majopo ya wataalam waliotoa mwelekeo wa kukabiliana na tatizo hilo.
Anasema kukosekana kwa mwafaka wa mpito kati ya serikali ya zamani na sasa, kumechangia kudorora kwa uchumi akieleza kuwa njia pekee ya kulinusuru taifa hili kutoka kwa hali hii ngumu ni kuwachana na siasa na kuyapa kipaumbele maswala ya kujenga nchi.
Shauri amesisitiza kuwa baraza la kushulikia uchumi nchini huenda likapoteza muelekeo iwapo litaendelea kujihusisha na siasa na kulalamika badala ya kutoa ushauri kwa rais William Ruto, kuhusu jinsi ya kukabiliana na hali ngumu ya kudorora kwa uchumi.
BY ERICKSON KADZEHA.