HabariNewsSiasa

Odinga aendelea Kuipinga Sheria ya Fedha 2023, Akisema si Salama kwa Uchumi na Wawekezaji

Kinara wa mrengo wa AZIMIO la Umoja Raila Odinga anaendelea kuipinga sheria ya fedha ya mwaka 2023 akikariri kuwa si nzuri na itazidi kuwakandamiza Wakenya na hata kuwafurusha Wawekezaji nchini.

Akihutubia wanahabari katika Jumba la Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga, Raila amesema tayari wawekezaji wameanza kuondoka nchini kuhamia mataifa mengine wakihofia matozo ya ushuru.

Odinga amesema kuwa ada za kuendesha biashara kwa wawekezaji zitapanda zaidi na kuwafukuza wawekezaji mbali, akisema kuwa imekuwa afueni na rahisi mno kuendesha biashara ya uwekezaji na uzalishaji nchini Misri kuliko hapa nchini.

“Sheria hii ya ushuru itaongeza ada za kuendesha biashara nchini na kuwaumiza Wakenya. Katika historia ya utengenezaji wa bajeti Kenya hakuna uongozi uliowahi kuongeza ushuru kupita kiasi kama ilivyo kwa serikali hii, Sheria hii ni ya kukandamiza uchumi na wawekezaji na inapaswa kukataliwa kwa kila namna,” akakariri Odinga.

Aidha Odinga amesema Muungano wa Azimio utatoa maelekezo zaidi kwa wabunge wake ambao wanatarajiwa kuwasilisha hoja bungeni kupinga mapendekezo kadhaa yaliyojumuishwa kwenye sheria ya fedha.

Viongozi wengine waliokuwa kwenye mkutano huo ni Kinara wa WIPER Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa Usawa kwa Wote Mwangi Wa Iria, Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Kiongozi wa Roots Party George Wajackoya, Peter Munya wa PNU na katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni pamoja na aliyekuwa Gavana wa Laikipia Nderitu Muriithi.

Kwenye mkutano huo viongozi hao wameunga mkono kamati inayoongozwa na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka itakayoongoza mazungumzo na serikali.

BY NEWS DESK.