LifestyleMombasaNews

WAZAZI NA WACHUNGAJI WATAKIWA KUWALEA WATOTO KATIKA MISINGI YA KIDINI.

Wazazi na wachungaji wametakiwa kuwashauri na kuwalea watoto katika misingi ya kidini ili kuhakikisha kuwa hawapotokwi kimaadili. Haya ni kutokana na idadi kubwa ya vijana kuripotiwa kujihusisha na utumizi wa dawa za kulevya maeneo mengi ukanda wa pwani.

Utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana unaendelea kuwa changamoto kubwa maeneo mengi ukanda wa pwani na sasa mikakati ya kukabiliana na hali hiyo inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa wadau  mbali mbali wakiwemo viongozi wa kidini.

Kwa mujibu wa Reuben Lewa mchungaji wa makanisa ya PEFA kaunti ya Kilifi viongozi wa dini wanafaa kuwashirikisha watoto kwenye ibada na kuwaombea badala ya kuwaangazia watu wazima na wale walio na uwezo wa kifedha pekee,  jambo analosema limepelekea vijana wengi kupotea.

“Huduma ya makanisa ile watu wote. Wakati mwingi huduma zinalenga watu wazima,wakati mwengine pia tunalenga wale wenye uwezo wa kihela lakini hata Yesu mwenyewe alisema, alipomwambia Petro kwamba lisha wanakondoo, halafu akasema chunga kondoo, halafu akasema lisha kondoo. Sasa inaanza na watoto. Watoto wengi wametelekezwa kwa hivyo watoto ni walelewe katika njia za maadili na tena waombewe na pia wazazi wawafuatilie.” alisema Lewa

Kwa upande wake mhadhiri wa chuo kikuu cha Pwani Profesa Chenje Mwachiro amesema hali ya umasikini ni miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia kuongezeka kwa visa vya utumizi wa dawa za kulevya.

Aidha amewataka wazazi kukoma kutumia dawa hizo mbele ya watoto kwani huiga mfano kutoka kwa wazazi jambo analodai huchochea watoto kujaribu kisha kujikuta wamenaswa kwenye mtego huo.

 “Kuna wazazi wengine pia wanatumia mihadarati kwa hivyo motto akiona kwamba hata baba anatumia anaingiwa na moyo wakuendelea kutumia ile mihadarati na kuona ni kitu cha kawaida. Kwa hivyo tuanze na sisi wazazi kuwashauri watoto. Jambo lengine labda nyumbani hakuna kitu wazazi wanasema katafute kitu fulani nap engine hawezi kupata wakati mwengine pia inakuja kwa msongo wa mawazo.” alisema Chenje.

 

ERICKSON KADZEHA.