HabariKimataifaNews

Rais Ruto Aomboleza Kifo cha Rais wa Iran, Ebrahim Raisi

Rais William Ruto mnamo Jumatatu Mei 20 alijiunga na viongozi wenzake duniani kutuma risala za rambirambi kwa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi ambaye aliaga dunia kutokana na ajali ya ndege

Kwenye ujumbe wake kupitia mtandao wa X rais William Ruto amemtaja kiongozi huyo kama mchapakazi aliyejituma katika nchi yake huku akiongeza kwamba ni pigo na pengo kubwa kwa Nchi ya Iran.

Raisi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 63 akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Nchi hiyo Hossein Amir Abdollahi pamoja na viongozi wengine.

Kulingana na Kituo cha habari kilicho na mafungamano na jeshi la ulinzi la mapinduzi la taifa la Kiislamu la Irani, Tasniim kimeripoti kuwa mazishi ya Rais Ebrahim Raisi yatafanyika Jumanne Mei 20 huko eneo la Tabriz mji uliokuwa akisafiria kabla mkasa kutokea.

Imeripotiwa kuwa pia mazishi mengine ya watu waliofariki yatafanyika Jumanne Mei 20.

Tayari Kiongozi wa Juu wa Kisiasa na Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alimtangaza makamu wa kwanza wa rais Mohammad Mokhber kuwa Kaimu Rais.

Mokhber aliongoza kikao chake cha kwanza cha baraza la mawaziri akihakikishia raia wa taifa hilo kuwa hakuna kitakachoharibika baada ya kifo cha Ebrahim Raisi.

“Hili ni tukio zito la kusikitisha kwetu sote. Linasababisha huzuni na uchungu lakini kuhusu suala la utawala na mwenendo wa nchi, watu wote wanapaswa kuwa na uhakika kuwa hakutakuwa na tatizo lolote.” Alisema Mohammad Mokhber.

BY NEWS DESK