KimataifaNews

Zuma Hastahili Kugombea Katika Uchaguzi Mkuu Afrika Kusini

Mahakama ya Afrika Kusini imeamua kuwa rais wa zamani wa taifa hilo Jacob Zuma hawezi kugombea kiti cha ubunge katika uchaguzi ujao mwezi huu.

Uamuzi huo uliotolewa mapema Jumatatu Mei 20 na mahakama ya Katiba umeafiki uamuzi wa awali wa mwezi Machi wa Tume ya Uchaguzi ya taifa hilo uliombandua Zuma katika mchakato wa kuwania wadhfa huo.

Mahakama hiyo imeshikilia uamuzi wa Tume hiyo wa kutomuidhinisha Jacob Zuma kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu na kwamba katiba ya Afrika ya Kusini inatoa katazo kwa mtu yeyote kugombea ikiwa amewahi kufungwa jela kwa zaidi ya miezi 12 au zaidi.

“Inatangazwa kuwa Bwana Zuma alitiwa hatiani kwa kosa na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 na kwa mujibu wa katiba ni kwamba hastahili kugombea katika uchaguzi mkuu.” Ulisema uamuzi wa Mahakama.

Mnamo mwaka 2021 Zuma alifungwa kifungo kifungo cha miezi 15 jela kwa kushindwa kufika katika kikao cha kesi ya ufisadi.

Itakumbukwa uhusiano kati ya chama tawala ANC na Jacob Zuma ambaye alilazimika kujiuzulu kama rais mnamo mwaka 2018 uliingia ufa na amekuwa akikifania kampeini chama kipya cha uMkhonto we Sizwe chama ambacho kimeonekana kuwa tishio kwa chama tawala.

Zuma aliyekuwa rais wa Afrika Kusini kuanzia 2009-2018 alijiuzulu katika nafasi hiyo kwa tuhuma za ufisadi ingawa mwishoni mwa mwaka uliopita alirudi tena kwenye ulingo wa kisiasa akiwa na chama kipya cha uMkhonto we Sizwe MK na amekuwa akikosoa vikali chama chake cha zamani cha ANC ambacho amewahi kukiongoza.

 

BY NEWS DESK