Kwa mara nyingine tena Rais William Ruto amesisitiza msimamo wa dhidi ya maandamano ya vurugu, akisema Serikali yake haitaruhusu vurugu na ghasia za aina yoyote kutawala na kuvuruga amani ya taifa.
Akiongea siku ya Alhamisi 3 Agosti, katika Mji wa Konza kaunti ya Machakos wakati wa hafla ya ufunguzi wa Chuo Kikuu cha Kidijitali cha Open University of Kenya (OUK) rais Ruto amesisitiza kuwa hataruhusu ghasia kutumika kuigawanya na kuharibu nchi akibaini kuwa serikali yake itasimama imara kusimamia haki.
“Liwe liwalo tutatumia raslimali tulizo nazo kuhakikisha usalama wa maisha ya Wakenya, mali na biashara zao, kuhakikisha Kenya iko imara katika msingi wa nchi salama ya amani.” Alisema Rais.
Ruto amesema kuwa serikali yake iko imara kusimamia rasilimali na kulinda maisha ya Wakenya na biashara ili kuhakikisha taifa liko katika msingi imara wa demokrasia na wenye amani.
“Vurugu zinahujumu demokrasia yetu, vurugu zinahujumu maendeleo yote na ukuaji wa taifa, hivyo hatuwezi kuruhusu kamwe,” akakariri rais.
Wakati huo huo rais amesema kuwa hawawezi kuomba fedha kila mara kwa nchini zengine ila kujitegemea kama taifa na kuhakikishia wakenya kuwa rasilimali watakazo toa zitalindwa na serikali yake.
“Hatuwezi kuwa nchi inayokopa na nawashukuru wakenya kwa kuniambia kwa ufanisi wako tayari kuchangia kuhakikisha tuna rasilimali lakini wamesema nihakikishe rasilimali hizo zisiibiwe na mtu yeyote.” Alisema Ruto
Katika hafla hiyo Rais alibaini kuwa Serikali imejitolea kuongeza upatikanaji wa elimu kwa gharama nafuu na bora nchini.
Rais Ruto amesema utawala wake una nia ya kutoa elimu yenye ushindani na inayolenga kutosheleza mahitaji ya tasnia, kulingana na ajenda ya Serikali ya mabadiliko ya kiuchumi.
Alibainisha kuwa lengo ni kuwezesha asilimia 100 ya mpito kutoka shule za upili hadi elimu ya juu.
Kiongozi wa Nchi alikuwa akizungumza siku ya Alhamisi huko Konza wakati wa kukabidhi Hati kwa Chuo Kikuu cha Kidijitali cha Open University of Kenya (OUK).
Hiki ni chuo kikuu cha kwanza cha mtandao cha umma nchini.