HabariNews

Mikakati kabambe yawekwa kukabiliana na tatizo la afya ya akili kaunti ya Kilifi

Kaunti ya Kilifi Serikali ya Kaunti ya Kilifi imeweka mikakati kuhakikisha kuwa inakabiliana kikamilifu na masuala ya afya ya akili kaunti hiyo.

Hatua hiyo inajiri kufuatia ripoti ya shirika la afya duniani WHO, kubaini kuwa Kenya inashikilia nafasi tano barani Afrika kwa idadi kubwa ya visa vya watu kukumbwa na msongo ya mawazo ambavyo vimesababishwa na matatizo ya afya ya akili.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa masuala ya Utamaduni, Jinsia na Huduma za Kijamii kaunti ya Kilifi Agneta Karembo, kunayo mikakati ambayo tayari mingine inaendelezwa kama kinga na suluhu la muda mfupi.

Amesema, idara yake imeanzisha mafunzo ya washauri wa kijamii katika viwango vya wadi zote 35 za kaunti ya Kilifi ambapo wamewafunza takriban washauri wa nyanjani 58 watakaokuwa na jukumu la kutoa ushauri nasaha kwa watu katika maeneo yao ili kupunguza idadi ya watu ambao huenda wanakabiliwa na matatizo ya akili.

 

“Tumeanza mafunzo ya washauri wa afya ya akili kutoa ushauri nasaha ya msingi katika ngazi za wadi zote eneo hili. Kwa sasa tushawapa mafunzo maafisa 58 na tutaendelea ili mtu akipatikana na shida kule nyanjani anajua kuna mtu ama afisa pale anayeweza kumsupport,” akasema Bi. Karembo.

Alongeza kuwa mbali na hayo, kuna sera ambazo zimependekezwa kupitia sekta ya afya ili kusaidia katika kutegua changamoto hii.

Amesema wanashirikiana na wadau mbalimbali ikwemo shirika la FIDA na mashirika mengine ya kimataifa katika kutekeleza mikakati hiyo.

“Tuna sera ya afya ya akili katika Idara ya afya tunashirikiana kuikuza hadi itakapopitishwa ili tuwe tunaitumia. Kuna namba iwapo mtu ana shida anaweza kupiga kueleza matatizo na kusaidika, kuna wengi wana matatizo ila sasa wanashindwa kueleza,” alikariri Karembo.

 

Haya yanajiri katika kipindi ambacho kumeshuhudiwa visa vya watu kujitoa uhai kwa kujirusha kwenye daraja la Kilifi katika siku za hivi karibuni.

BY ERICKSON KADZEHA