HabariNewsSiasa

Pasta Ezekiel adai kuwepo Njama ya Serikali Kumhangaisha

Mhubiri wa kanisa la New Life Prayer Centre and Church Ezekiel Odero amekashifu hatua ya serikali kubatilisha usajili wa kanisa lake akiitaja kama mbinu ya kumhangaisha.

Kupitia wakili wake Dnstan Omare Pasta Ezekiel, ameitaka mahakama ifutilie mbali uamuzi wa kubatilisha leseni ya usajili wa kanisa lake akisema uamuzi huo unakiuka uhuru wa kuabudu.

Kwenye hati kiapo ambayo iliwasilishwa na wakili katika mahakama ya Milimani, kasisi Odero amelalamika kwamba hakupewa nafasi ya kujitetea kabla ya msajili wa mashirika kufutilia mbali usajili wa kanisa lake.

Odero amesema kwamba alipata ujumbe kuhusu notisi kutoka kwa mahakama kupitia vyombo vya habari siku nane baada ya kumalizika kwa ilani iliyokusudiwa ya siku 21.

“Mpango ulioandaliwa na Mhojiwa wa 1 wa kughairi usajili wa kanisa tarehe 19 Mei 2023 na kuchapishwa tarehe 18 Agosti 2023, lakini Mwombaji alijua tu notisi ya kuonyesha sababu mnamo tarehe 25 Mei 2023, ni katika nia ya kukatisha tama na kumnyima Mwombaji haki ya kupata hatua za kiutawala  kwa kuzingatia mkutano wake ujao wa kimataifa wa ‘Meza ya Bwana’, uliopangwa kufanyika kwa muda wa siku 14,” ilisema taarifa hiyo ya Korti.

Odero amedokeza kwamba iwapo mahakama haitaingilia kati atapata madhara yasiyoweza kurekebishwa na uhuru wa waumini wake wa kuabudu utaminywa kinyume cha Kifungu cha 32 cha Katiba.

Odero sasa amemtaka Mwanasheria Mkuu wa serikali Justin Muturi kuweka wazi sababu zilizompelekea kuteleza hatua hiyo.

Kanisa la New Life Prayer Centre and Church ni miongoni mwa makanisa yaliyopokonywa leseni pamoja na kanisa la Kings Outreach linaloongozwa na nabii David Owuor.