HabariNews

Waziri Kindiki: Ufisadi jumba la Nyayo umechangia Ugaidi na Utovu wa Usalama

Miongoni mwa matatizo yanayokumba taifa ikiwemo ukosefu wa usalama na visa vya ugaidi nchini yanatokana na utepetevu na ufisadi uliokithiri katika Jumba la Nyayo house jijini Nairobi.

Haya ni kwa mujibu wa Waziri wa masuala ya Ndani na Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki.

Akiongea mbele ya Kamati ya bunge kuhusu Ushirikiano wa Kikanda Agosti 24, 2023, Waziri Kindiki aliapa kukabiliana vilivyo na ufisadi unaohusishwa na maafisa wa idara ya uhamiaji katika jumba hilo.

Ukienda Wajir, vijana wa miaka 21 wanasubiria Vitambulisho kwa miaka 3 sasa,” alisema Kindiki.

Kindiki aidha alikiri kuwepo kwa ufisadi miongoni mwa maafisa ambao huchelewesha mchakato wa utengenezaji na utoaji wa paspoti kwa kuitisha hongo kwa ajili ya huduma ambazo serikali hutoa bila malipo.

Amebaini kuwa Jumba hilo la Nyayo kwa sasa ni eneo la uhalifu akiahidi kulifunga Jumba hilo ili kulisafisha kutokana uozo huo wa ufisadi.

Nitalisafisha jumba la nyayo mara moja. Tutalifunga jumba la nyayo na kulitaja kuwa eneo la uhalifu. Haitakua biashara kama kawaida, lazima tulisafishe jumba hili,” alisema.

Kulingana na Kindiki pasipoti zinazopaswa kushughulikiwa kwa sasa ni 58,000, huku Idara ya Uhamiaji na Huduma za Raia ikitengeneza takribani paspoti 5,000 kila siku.

Kindiki hata hivyo aliahidi kuwa mipango kabambe ya kuhakikisha paspoti zinatolewa katika muda wa siku 7 na kudokeza kwamba katika siku zijazo, muda wa utoaji vyeti hivyo utapunguzwa hadi siku 3  na saa 24 kunapokuwa ombi au tukio la dharura.