Wawekezaji 3 wamesalimisha kwa tume ya maadili na kupambana na rushwa nchini EACC vipande vitatu vya ardhi kaunti ya kwale vyenye thamani ya Shilingi milioni 305.
Kulingana na EACC, vipande hivyo vinavyomilikiwa na shirika la kuhifadhi wanyama pori nchini KWS, vilipatikana kupitia kwa utaratibu mbadala wa shirika hilo kutatua mizozo ADR. Utaratibu huo unaleta pamoja watu wanaomiliki mali ya umma katika mazungumzo na EACC ili kujisalimisha kwa hiari na kuepukana na gharama iwapo kesi itafika kotini.
“Tume inawahimiza watu wengine wote wanaomiliki mali ya umma kinyume cha sheria kutumia fursa ya utaratibu wa ADR kutatua migogoro badala ya kusubiri mchakato mrefu na wa gharama kubwa ya kesi”
Mkuu wa mawasiliano EACC Erick Ngumbi alisema kuwa kabla ya kupatikana kwa ardi hizo, moja kati yao ilitengewa ujenzi wa uwanja binafsi wa ndege.
EACC hata hivyo ilithibitisha kuwa Pwani Holdings Resort, Bantus Investments pamoja na Pangos walikubali kurudhisha ardhi hizo na kusalimisha stakabadhi za umiliki huku mikakati ya kupata sehemu zilizosalia ikiendelea
Swali kuu linalosalia kwa tume hii , ni kwanini sehemu hizo zilisajiliwa kwa majina ya watu binafsi hali ya kuwa inamilikiwa na shirika la KWS? Hili limepelekea Ngumbi kuitisha uchunguzi Zaidi huku akiwataka wahusika wanasalimisha ardhi hizo kupitia mazungumzo ADR
“Ugawaji wa ardhi hii kwa watu binafsi haukuwa halali na ulaghai kwa vile imetangazwa kwenye gazeti la serikali kama Kisite Hifadhi ya Taifa ya Mpunguti na Hifadhi.” Ilisema EACC
Eacc kwa sasa imeelekea kotini kupigania mali zilizopatikana kulaghai zenye gharama ya takriban shilingi bilioni 8, Mombasa ikiongoza kwa kesi za unyakuzi wa ardhi.