Mahakama ya kukabiliana na ufisadi nchini imeiamuru EACC kutoa vifaa au stakabadhi zozote zisizohusiana na kesi ambayo inamhoji aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini EACC ilikuwa imepata hati za upekuzi na kukamata vitu mbalimbali vya Oparanya vinavyohusishwa na madai ya kupatikana kwa mali kwa njia isiyofaa.
Katika ombi lililowasilishwa kortini Oparanya alisema kuwa maafisa wa EACC walivamia na kuchukua hati, kompyuta, simu za rununu pamoja na pesa taslimu Sh2 milioni. Oparanya alidai kuwa Msako huo haukuidhinisha maafisa hao kukamata na kubeba hati yoyote bila kuonyesha uhusiano kati ya hati hizo na uhalifu wowote unaodaiwa.
“Amri hizo hazikuidhinisha mtu yeyote kukamata na kubeba simu zozote za rununu na kompyuta za watu wengine ambao hawakushiriki katika kesi hiyo,” Oparanya alisema.
Kulingana na Oparanya, EACC ilivuka mipaka ya maagizo ya mahakama walipowanyang’anya watoto wake, wake zake na wafanyikazi wake simu za rununu. Hata hivyo hakimu Mkuu Thomas Nzyuki aliagiza upande wa mashtaka na mawakili wanaomwakilisha Oparanya wafanye mkutano wa pamoja na kuafikiana kuhusu stakabadhi zinazofaa kwa kesi hiyo ili zihifadhiwe.