HabariNews

“Nitajitahidi kuunganisha Waumini” Kadhi Mkuu Asema

Nitajitahidi kuleta umoja kwa kuunganisha madhehebu mbali mbali na umma wa Kiislamu kwa ajili ya ushirikiano na maendeleo.

Ni kauli yake Kadhi Mkuu mpya nchini Sheikh Abdulhaleem Hussein Athman, ambaye alibaini kuwa migawanyiko inayoshuhudiwa imekuwa kikwazo kwa maendeleo kabambe kwa jamii ya waislamu nchini.

Akiongea katika Dhifa la heshima la kumkaribisha kwake lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu nchini SUPKEM, Kadhi Mkuu huyo alibaini kuwa ushirikiano ndio utakaofanikisha maendeleo ya jamii ya waislamu nchini.

“Naamini tukishirikiana tutafanikiwa zaidi, nitafanya kila juhudi kwa ushirikiano na wenzangu kuleta umoja na kuunganisha jamii ya waislamu nchini bila kuzingatia tofauti ya madhehebu ya dini,” alisema Kadhi Mkuu.

Vile vile Sheikh Abdulhaleem aliapa kukabiliana na ufisadi katika afisi yake hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa makadhi mafisadi wanaolemaza shughuli na hata kuifanya afisi yake kukosa heshima.

Kwa upande wake naibu Mwenyekiti wa kitaifa wa SUPKEM Sheikh Muhdhar Khitamy aliwausia waumini wa Kiislamu kushikamana na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kushirikiana sawia na kuiheshimu afisi ya Kadhi Mkuu.

“Qur’an inatwambia tushikamane kwa kamba ya Allah wala tusifarikiane na kutengana. Na tutakapokuwa na matatizo turudi kwake Mola na Mtume wake. Nawausia wenzangu tuungane na tushirikiane na Kadhi wetu huyu kwa manufaa yetu sote,” alisema Sheikh Khitamy.

Wakati huo huo Sheikh Muhammad Dor wa Baraza la Maimamu na Wahubiti nchini CIPK alimtaka Kadhi Mkuu kufanya kila juhudi kuondoa migogoro na tofauti za za waumini zilizopo kwa kushughulikia suala la mvutano linalojitokeza wakati wa mwandamo wa mwezi wa Mfungo na Sikukuu ya Eid.

“Bwana Chief Kadhi nitasema tu ukweli familia nyingi zimekuwa kwenye mgogoro, majumba yamechafuka kwa kugawanyana linapofikia suala la mwandamo wa mwezi, mama, baba na watoto. Hili suala la tofauti limekuwa kikwazo hivyo afisi yako naomba itafute mbinu kushughulikia hilo.” Alisema Sheikh Dor.

Naye Sheikh Hassan Sugow alisisitiza umuhimu wa waumini kuunganishwa kupitia afisi hiyo ya Kadhi Mkuu ili kuepuka migogoro ya mwandamo ya mwezi katika siku za usoni.

Sheikh Sugow alibaini kuwa migogoro hiyo inayoshuhudiwa kila mwaka imekuwa changamoto na imefika wakati wa kuwaunganisha waumini.

BY MJOMBA RASHID