Serikali ya kaunti ya Mombasa inapania kuweka mikakati ya kubadilisha mabomba ya m aji ili kuimarisha na kuongeza kiwango cha maji kwa wakazi wa kaunti hiyo.
Kulingana na gavana wa Mombasa Abdulswamard Sharif Nassir kiwango cha maji kinachohitajika kaunti ya Mombasa ni takribani cubic mita laki 2 illhali maji yanayoingia katika kaunti hii ni cubic mita elfu 50.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa mradi wa maji huko Junda eneobunge la Kisauni uliogharimu takribani milioni moja gavana Nassir alisema mradi huo utasaidia wakazi wa Kisauni na Mombasa kwa ujumla kutokana na donda sugu la uhaba wa maji linaoendelea kushuhudiwa kwa wakaazi hao.
“Kwa ushirikiano na mashirika haya tunahitaji kupanua mabomba yetu haya kuongeza kiwango cha maji. Kwa sasa mita cubic mita elfu 50 kiwango tunachopata hakitoshelezi kaunti nzima,” alisema
Mradi huo kwa ushirikiano wa shirika la Give Power, serikali ya kaunti ya Mombasa na kampuni ya Service Now unatarajia kunufaisha wakazi takribani elfu 30.
“Ni mpangilio ambao unatoa maji, maji ambayo yameza kusafishwa lita elfu 75 ambao ni mita cubic 75. Ukipiga hesabu vile vile hii itaweza kusaidia sana, ina uwezo kusaidia watu takribani elfu 30,” alisema gavana Nassir.
Kwa upande wake waziri wa maji kaunti ya Mombasa Emily Achieng ameutaja mradi huo utakaowanufaisha sio wakaazi wa kisauni bali Mombasa yote kwa ujumla aidha amesema yuko tayari kushirikiana na washikadau mbalimbali ili kuhakikisha shida ya maji mjini Mombasa imetatuliwa vilivyo.
Haya yanajiri ikiwa serikali ya kaunti ya Mombasa ikiwa na vituo vinne tu vyenye mradi wa maji.