MAAFISA kadhaa katika Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF) wamepoteza maisha baada ya ndege waliokuwa wakiabiri kuanguka msituni Boni, kaunti ya Lamu.
Akithibitisha tukio hilo Jumanne, Msemaji wa Idara ya Jeshi, Brigedia Zipporah Kioko alisema kuwa ndege aina ya helikopta iliyokuwa imebeba maafisa waliokuwa wakishika doria za anga katika msitu huo ilianguka Jumatatu usiku..
Kulingana na Brigedia Kioko, wanajeshi waliofariki katika ajali hio ni miongoni mwa wale wanaoendeleza operesheni ya Amani Boni inayolenga kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.
Operesheni hiyo ilizinduliwa na serikali kuu mnamo Septemba, 2015 na imekuwa ikiendelezwa kwenye kaunti za Lamu, Tana River, Garissa na Kilifi.
“Tunasikitika kutanganza kwamba helikopta ya wamajeshi wa kikosi cha angani ilianguka usiku wakati wanajeshi walikuwa wakishika doria za angani kwenye operesheni inayoendelea ya Amani Boni huko Lamu. Tunatoa rambirambi zetu kwa jamaa, familia na marafiki wa wanajeshi wetu waliopoteza maisha,” alisema Brigedia
Hata hivyo idadi ya walinda usalama walioangamia kwenye ajali hiyo ya ndege na pia sababu zilizopelekea helikopta hiyo kuanguka haikufichuliwa.
“Jopokazi maalum la kuchunguza ajali hiyo ya ndege limeundwa na kutumwa Lamu ili kutafiti na kubaini kilichosababisha ndege hiyo kuanguka. Maelezo ya ziada ni baada ya jopokazi kukamilisha uchunguzi wake,” akasema Brigedia Kioko.
Ajali hiyo ya ndege ya kijeshi inajiri siku tatu tu baada ya KDF kuwaua washukiwa wa kundi la Al-Shabaab na kunasa sihala mbalimbali eneo la Bodhei ndani yam situ wa Boni, kaunti ya Lamu.
Uvamizi huo kwenye maficho mawili ya Al-Shabaab ulitekelezwa na KDF Jumamosi usiku punde walipopata taarifa za kijasusi kuhusu kuonekana kwa magaidi wa kundi hilo eneo hilo la Bodhei.