HabariNews

Kenya haiko katika hali mbaya vile! Yasema Kenya Kwanza

Viongozi wa Kenya Kwanza wametoa mwanga wa matumaini kwa Wakenya wa kuimarika kwa uchumi na kushuka kwa gharama ya maisha nchini.

Hii linajiri ni licha ya kushuhudiwa ongezeko la bei ya mafuta nchini na kuzua hofu ya kupanda zaidi kwa gharama ya maisha.

Akizungumza kwenye Kongamano la Kamati teule la Wabunge kuhusu utekelezwaji wa Bajeti mjini Mombasa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti bungeni Ndindi Nyoro alidai kuwa taifa la Kenya halipo katika hali mbaya sana kiuchumi kama inavyodaiwa na kwamba serikali i mbioni kutekeleza mikakati yake ya kuimarisha hali ya uchumi.

Licha ya ongezeko hilo la mafuta na kupanda kwa gharama ya maisha Nyoro alieleza matumaini ya kushuka kwa bei za bidhaa.

“Kenya haiko katika hali mbaya sana vile, tunajaribu kila tuwezalo kuimarisha hali ya uchumi. Nataka kuwahakikishia wakenya kuwa tunafanya kila tuwezalo kuimarisha hali. Linapokuja suala la mafuta, suala la kwanza ni bei zake lakini muhimu zaidi na hata mbaya ni upatikanaji wake, tufahamu hata katika mataifa mengine jirani baadhi ya maeneo hakuna mafuta kabisa,” alisema Nyoro.

Kwa upande wake Mdhibiti Mkuu wa Bajeti Bi. Margaret Nyakang’o ukubwa wa deni  humu nchini ulisababishwa na kupungua kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya Dola ya Marekani. Nyakang’o aidha ameongeza kuwa bilioni 1.8 imetengwa kwenye bajeti ya mwaka elfu 2023-2024 kama ruzuku ya mafuta.

Mdhibiti huyo hata hivyo alipendekeza serikali kutumia sarafu nyingine ya fedha iwapo watakopa katika mataifa ya ng’ambo.

“Ripoti tulizozipata kutoka kwa Hazina yetu ya Kitaifa ilionyesha kuwa deni letu kufikia Juni 30 lilikuwa trilioni 10.25 ambayo ni kubwa sana kiwango cha kisheria. Ila nisisitize kuwa sehemu ya deni hili ni kutokana na kupanda kwa kiwango cha ubadilishaji wa sarafu za kigeni, sote tunajua shilingi kufifia na kukosa thamani mbele ya dola,” alisema Bi. Nyakang’o.

BY EDITORIAL DESK