HabariNews

Kikosi Spesheli Kutumwa Kuzima Ugaidi Tana River Na Lamu

Kenya itatuma kikosi spesheli cha wallinz wa usalama katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi, ukanda wa juu wa pwani kukabiliana na magaidi. Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki alithibitisha haya akiwa katika eneo la Wayu, Galledyertu katika Kaunti ya Tana River.

“Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba maafisa wetu wanapata silaha vifaa vya kiteknolojia vitakavyowapa uwezo wa kukabiliana na wahalifu,” amesema waziri Kindiki akiahidi kwamba wanaotumia silaha ipasavyo ili kujilinda nao wataendelea kuungwa mkono kikamilifu.

Kindiki alizitaka jamii jirani kuendelea kuishi bila kuzozana na endapo kutatokea mgogoro basi waachie serikali pamoja na  taasisi huru kama idara ya mahakama fursa ya kutatua kesi.

Waziri huyo alisema kuanzia Oktoba 1, 2023, serikali itatuma mwanakandarasi kujenga makao ya utawala katika eneo la Galledyertu huku akitoa wito kwa maafisa wa utawala kuhakikisha wanatekeleza kazi yao kwa uadilifu bila kuegemea upande wowote.

Viongozi mbali mbali hatahivyo akiwemo Gavana wa Tana River Godhana Dhadho, Seneta Danson Mungatana, wabunge, madiwani na mshirikishi wa pwani pamoja na kamati za kiusalama wamehudhuria kikao cha baraza kuangazia suala la usalama.

Kauli ya waziri huyo inajiri tu baada ya shambulio kutokea katika eneo la Widho-Mashambani, Lamu Magharibi ambapo bawabu mmoja aliuawa na Al-Shabaab walioteketeza takribani nyumba tano.

BY EDITORIAL DESK