HabariTravel

Fungueni Anga la Mombasa! Wadau wa Utalii walilia Serikali Kuu

Ili kuimarisha viwango vya utalii kaunti ya Mombasa na Pwani kwa jumla, Serikali Kuu inapaswa kurejesha kikamilifu mfumo wa anga huru kwa haraka iwezekanavyo.

Ni kauli yake Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nasser, akiongea katika Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yaliyofanyika katika Bustani la Treasury Square, mnamo Jumatano Septemba 27.

Akiongea katika maadhimisho hayo Gavana Nasser alikariri kuwepo haja ya serikali kutekeleza mfumo huo wa (Open Sky policy) kwa kuruhusu kikamilifu safari za moja kwa moja za ndege za kimataifa kuja mjini Mombasa ili kuimarisha viwango vya utalii.

“Tunasisitiza ufunguzi wa anga huru na kufunguliwa kwa anga huru haitastawisha Mombasa pekee bali kila kaunti kwa hivyo ni ombi langu na ni jambo ambalo linahitaji ushirikiano.” Alisema Nassir.

Wakati huo huo Gavana Nassir aliitaka serikali kuondoa matozo kwa meli zinazoingiza mizigo na abiria bandarini akisema hatua hiyo itavutia watalii wengi zaidi nchini ili kukuza uchumi wa taifa.

“Sisi tunaomba serikali iweze watoe mambo ya visa, tunataka wale watalii watoke, waingie na waende katika hoteli zetu wale vyakula vyetu na kuangalia historia zetu kwenye vivutio vyetu.” Aliongeza Gavana Nassir.

Sam Ikwaye ambaye ni Afisa Mtendaji wa Muungano wa Wamiliki wa Hoteli za Kitalii Pwani, alibaini kuwa sekta ya utalii ukanda wa Pwani imeanza kuimarika kutokana na ongezeko la wageni wanaozuru maeneo hayo.

Ikwaye alisisitiza haja ya kufunguliwa kwa anga huru akisema kuwa hatua hiyo itasaidia sekta hiyo kwa kiwango kikubwa.

“Kumekuwa na ongezeko la wageni hasa mwaka jana na mwaka juu hapa eneo la Pwani na hususan tunasisitiza kufunguliwa kwa anga huru ili tuweze kupiga jeki shughuli za kitalii vile vile tumeona kuna ongezeko la uwekezaji katika sekta hii.” Alisema Ikwaye.

Haya yanajiri huku Kenya ikiungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani ambayo huadhimishwa Septemba 27 kila mwaka, Kauli mbiu ya maadhimisho yam waka huu ikiwa ni ‘Utalii na Uwekezaji katika utunzaji wa Mazingira,’ (Tourism & Green Investment).

BY MEDZA MDOE.