HabariLifestyleNews

Ongezeko la mafuta Tishio kwa Utalii! Watalii kugharamikia ada zaidi Pwani

Muungano wa wamiliki wa hoteli za kitalii eneo la Pwani umedokeza kuwa huenda ukalazimika kupandisha ada kwa wateja wao iwapo bei ya mafuta itaendelea kupanda.

Akizungumza na wanahabari pambizoni mwa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani katika Bustani ya Treasury Square mjini Mombasa, Afisa Mtendaji wa muungano huo Sam Ikwaye alisema mwaka ujao wataangalia upya ada zao kutokana na ongezeko la bei za bidhaa na huduma mbalimbali.

“Ni kweli bei za mafuta zimeenda juu hii ikimaanisha gharama za ada za usafiri pia zitaenda juu, na tayari tumeona kampuni kadhaa za ndege na wadau wengine wa uchukuzi tayari wakibadili viwango vyao vya malipo. Shughuli za raslimali za hoteli ni kama maduka ya jumla, hatuzalishi tunachokiuza,” alisema Ikwaye.

Ikwaye alisema kinachowazuia kwa sasa kutopandisha ada zao ni mkataba uliopo lakini watalazimika kufuata mkondo mwengine wa ada mpya mwaka ujao.

“Ni kweli kufahamu hapa kuwa mwaka unaokuja baada ya mkataba huu tulio nao tutakagua upya ada zetu kama sekta ya utalii ili tuweze kuakisi na kwenda sambamba na kuongezeka kwa gharama ya kufanya biashara.” Alisema Ikwaye

Hata hivyo Ikwaye alisisitiza haja ya mfumo kamili wa kufunguliwa kwa anga huru (Open sky Policy) mfumo utakaoruhusu ndege za moja kwa moja za kimataifa kuwasili mjini Mombasa, akisema kuwa hatua hiyo itasaidia sekta hiyo kuimarika kwa kiwango kikubwa.

“Kumekuwa na ongezeko la wageni hasa mwaka jana na mwaka juu hapa eneo la Pwani na hususan tunasisitiza kufunguliwa kwa anga huru ili tuweze kupiga jeki shughuli za kitalii vile vile tumeona kuna ongezeko la uwekezaji katika sekta hii.” Alisema Ikwaye.

Haya yanajiri huku Kenya ikiungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani ambayo huadhimishwa Septemba 27 kila mwaka, Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ikiwa ni ‘Utalii na Uwekezaji katika utunzaji wa Mazingira,’ (Tourism & Green Investment).

BY MJOMBA RASHID