HabariNews

Ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya DBK kuwafaa wakazi kibiashara kaunti ya Mombasa

Serikali ya kaunti ya Mombasa imeahidi kushirikiana na taasisi za kifedha na wawekezaji mbalimbali ili kuimarisha uchumi wake.

Akizungumza katika hafla ya kuzindua rasmi tawi la kwanza la Benki ya Maendeleo nchini, DBK katika kaunti ya Mombasa, Waziri wa Fedha wa kaunti hiyo Evans Oanda alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuvutia washikadau mbalimbali kuwekeza katika kaunti hiyo na kuinua uchumi wake.

Aliongeza kuwa kufunguliwa kwa benki hiyo kutaleta ushindani katika sekta  hiyo jambo analolitajwa kuwa na uwezo wa kuimarisha zaidi uchumi wa kaunti hii.

“Hii benki italeta ushindani wa kibiashara na hiyo inamaanisha kuinua uchumi wetu, kuimarisha uchumi wa kaunti hii. Sisi kama serikali ya kaunti hapa Mombasa tutashirikiana na taasisi kama hizi na wawekezaji wote,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Johnson Kiniti aliwahakikishia  wakazi wa kaunti hii kuwa watashirikiana na serikali ya kaunti ili wapate huduma bora.

Vilevile Kiniti alisema kuwa benki hiyo itazingatia wananchi wenye kipato cha chini kwa kuwapa fursa ya kuhifadhi fedha zao pamoja na kuwapa mikopo ya nafuu ili kuwawezesha kujiimarisha kimaisha.

“DBK tutajali zaidi na kuangazia wananchi wa kipato cha chini, tutawapa fursa wawekeze nasi na tutawapa mikopo nafuu wajiendeleze kimaisha. Pamoja tutashirikiana kujengana na kuinuana kibiashara,” Alisema.

Tawi hilo la benki ya DBK katika barabara ya Moi mjini Mombasa, ni la kwanza kufunguliwa katika kaunti hiyo baada ya kuwa na matawi mengine katika jiji kuu la Nairobi nchini Kenya.

BY BEBI SHEMAWIA