HabariKimataifaNewsWorld

Vita vya Israel-Palestina: KEMNAC yalaani Marekani kuisadia Israel silaha kushambulia Palestina

Baraza Kuu la ushauri kwa Waislamu nchini KEMNAC limekashifu uamuzi wa Marekani kuwapiga jeki kisilaha taifa la Israel katika mapigano baina ya taifa hilo na Palestine.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo sheikh Juma Ngao walisema hatua hiyo imezidisha maafa kwa kuendeleza vita baina ya mataifa hayo mawili.

Viongozi hao Walieleza masikitiko yao kwa matukio nchini Palestine wakiwataja kina mama na watoto kama waathiriwa wakubwa wa vita hivyo.

Tunalaani vikali Marekani, Nato, Israel na Umoja wa mataifa kwa kushirikiana kuwafurusha Wapelestina katika nchi yao, vita hivi si vya Israil na Hamas bali ni vya Amerika ,Uingereza na UN wakimsukuma Muisraili kufanya mashambulizi dhidi ya Wapalestina maskini katika nchi yao, wanaoumia hapa ni kina mama, watoto na wazee wa pande zote,” alisema Sheikh Ngao.

Wakati huohuo waliitaka mahakama ya kimataifa ya jinai ICC kutoa amri ya kuwakamata Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, rais wa Marekani Joe Biden na Waziri wa ulinzi wa Israel Benny Gantz ambao walidaiwa kuwa ndio wanaosukuma na kufadhili vita hivyo.

Baraza hilo vile vile lilikosoa hatua ya Umoja wa Mataifa ya kusitisha kutoa misaada kwa waathiriwa nchini Palestine katika kipindi hiki kigumu.

Twataka ICC itoe arrest warrant imkamate Rais Joe Bidden,waziri mkuu wa Israil Neta Nyau na waziri wa ulinzi wa Israil lazima wakamatwe kwa kusaidia katika vita hivyo,kwa hiyo tunaomba umoja wa mataifa vita visimamishwe mara moja na misada ya chakula,maji na madawa iweze kupelekwa maeneo hayo,” alisema.

Kwa upande wake Sheikh Hassan Mubarak Katibu Mtendaji wa Baraza hilo alikosoa baadhi ya vyombo vikuu vya habari vya kimataifa kwa kile wanachosema ni kuegemea upande mmoja kwenye kuangazia taarifa kuhusiana na vita hivyo huku wakiwarai wanahabari wa humu nchini kuendeleza usawa wanapotekeleza majukumu yao.

Tunakemea baadhi ya vyombo vya habari vya Kimataifa kuficha ukweli na habari muhimu zaidi kuhusu vita hivi, na nyinyi wanahabari wa Kenya pia nawaomba muwe kati kwa kati muangazie ya ukweli kuhusu kule Palestina, msichukua upande wowote,” alisisitiza.

Haya yanajiri huku vita hivyo vilivyoanza majumaa kadhaa yaliyopita vikipelekea uharibifu wa mali na Wapalestina zaidi ya elfu 3 kupoteza maisha, na maelfu wakiachwa bila makao.

Shambulizi la hivi punde nchini Palestine likifanyika Usiku wa Jumanne kwenye hospitali na kupelekea watu takriban 500 kupoteza maisha.

BY BEBI SHEMAWIA