HabariNews

Wakuu wa shule za Msingi kusimamia Shule Msingi Sekondari (JSS), Serikali yasisitiza

Wizara ya elimu imetoa hakikisho kuwa walimu Wakuu wanaosimamia chekechea na shule za msingi ndio watakaoendelea na majukumu yao kuongoza shule za msingi sekondari (Junior Secondary) mwakani.

Akizungumza katika Kongamano la Walimu Wakuu wa shule za Msingi KEPSHA, linaloendelea hapa Mjini Mombasa, Waziri wa elimu Ezekiel Machogu hatimaye aliondoa hofu na sintofahamu iliyokuwepo, akisisitiza utekelezwaji wa ripoti ya Jopo Kazi la mtaala wa Elimu ya CBC.

Waziri Machogu alisema kuwa walimu wote wa shule za msingi walio na vyeti vya uzamifu kote nchini wanapaswa kupandishwa vyeo huku akidokeza kuwa Serikali imetenga shilingi Bilioni 1 kama nyongeza ya mshahara ili kutambua juhudi na utendakazi wao mzuri.

 

Kulingana na  Machogu serikali ikishirikiana na idara ya Elimu haitaruhusu mwalimu mkuu yeyote nchini kuongeza ada ya wanafunzi akisisitiza kuwa serikali imejipanga vizuri na kutoa onyo kwa walimu watakaofanya hivyo kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha Kitaifa cha Walimu nchini, KNUT Collins Oyoo hata hivyo aliitaja hatua hiyo  kuwapa motisha walimu wengi ambao wamehitimu na hawajatambulika vilivyo na serikali.

BY EDITORIAL DESK