HabariNews

Sakata ya Mafuta ya Bilioni 17: Je, Mfanyabiashara Ann Njoroge alighushi stakabadhi? Waziri Chirchir atoa taarifa

Serikali imekariri kuwa mfanyabiashara Ann Njeri Njoroge si mmiliki wa shehena ya mafuta ya thamani ya shilingi bilioni 17.

Wizara ya Kawi nchini imejitoa kimasomaso kupuuzilia mbali madai ya mfanyabiashara huyo aliyejitokeza baada ya kudai kutekwa nyara alipokuwa amefika makao makuu ya DCI kuandikisha taraifa kuhusu shehena hiyo.

Katika taarifa iliyotumwa chumba cha habari siku ya Jumatano, siku moja tu baada ya Anne kudai kuwa mmiliki wa mafuta hayo, Waziri wa Kawi Davis Chirchir alisema kuwa kampuni ya mfanyabiashara huyo iliyodaiwa kuagiza shehena hiyo haijaorodheshwa kama kampuni yenye leseni ya uagizaji mafuta.

Naweza kuwathibitishia kuwa kampuni ya Anns Import and Export Enterprises Ltd haijatia saini mkataba wa usafirishaji na uhifadhi kama inavyotakiwa chini ya Kanuni ya 6 ya Kanuni za Uagizaji wa Mafuta ya mwaka 2023, na hivyo haiwezi kuwa na sifa za kuwa kampuni ya uuzaji mafuta,” alisema Chirchir.

Kulingana na Waziri Chirchir kampuni ya mfanyabiashara huyo haijatia saini mkataba wa mfumo wazi wa zabuni na hivyo basi hawezi kudai kuwa ameingiza shehena ya mafuta ya dizeli nchini.

Waziri huyo aidha alifichua kuwa Kampuni ya Njeri ilituma maombi ya leseni ya kuagiza, kusafirisha na kuuza bidhaa za petroli kwa Mamlaka ya kudhibiti kawi na mafuta EPRA, kupitia tovuti ya mtandao mnamo Oktoba 9 2023.

Kwa mujibu wa Chirchir ombi lake hilo Njeri hata hivyo lilikataliwa siku 20 baadaye baada ya kutathminiwa kuwa kampuni hiyo ilishindwa kukidhi mahitaji.

Kampuni yake inadai kuwa leseni leseni ya kuagiza petroli ilitolewa, ikalipiwa na inasubiri kusainiwa jambo ambalo si kweli n ani uzushi kabisa,” aliongeza Waziri Chirchir.

Kwanza, kwa sasa EPRA haitozi ada za leseni za mafuta ya petroli na pili, EPRA haina katika rekodi zake leseni ya uingizaji wa mafuta ilitolea kwa Anns Import and Export Enterprises Limited ambayo inasubiri kusainiwa,”

Waziri huyo aidha alisema kuwa Wizara yake iliiandikia kampuni ya Aramco Trading Fujairah FZE ambayo ilituma maombi ya shehena hiyo kupitia kampuni ya uuzaji mafuta waliyoiteua ya Galana Energies Limited kwa usambazaji wa tani 85 za dizeli kuwasilishwa bandarini Mombasa kati ya Oktoba 17-19, 2023.

Alisisitiza kuwa meli hiyo ya MT Haigui ilikuwa imesheheni tani 93,460.46 za mafuta ya dizeli kutoka Bandari ya Yanbu Samref nchini Saudi Arabia, huku akipuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa tani laki moja za mfanyabiashara huyo.

BY MJOMBA RASHID