HabariNewsUncategorized

Wahudumu wa Bodaboda za Umeme Mombasa Waandamana Kulalamikia Ongezeko la Ada

Wahudumu wa BodaBoda zinazotumia umeme mjini Mombasa wameandamana nje ya kampuni ya Spiro eneo la Makupa wakilalamikia ongezeko la ada wanayotozwa na kampuni hiyo.

Wakizungumza na wanahabari mnamo Jumatatu, wahudumu hao walisema kampuni hiyo ya Spiro imeongeza ada ya kubadilisha betri kwa shilingi 75 na sasa wanatakiwa kulipa shilingi 290.

Wanabodaboda hao wameitaja hatua hiyo kwenda kinyume na maafikiano ya awali ya kulipa shilingi 215 kila wanapobadilisha betri za pikipiki zao.

 

Hatuwezi kukubali maana tulisaini mkataba na huo mkataba lazima tushirikishwe ndipo tuweze kuja mezani tuelewane kwa nini hii betri inaongezwa bei na kwa nini wanavunja mkataba ambao hatukuelewana,” alisema mmoja wa wahudumu hao.

Mwanabodaboda mwengine naye alisema, “Mkataba ulikuwa 215 kwa miaka 3, miezi miwili tu washakuja na mabadiliko wamebadilisha. Ndio kwa sababu tumeandamana , tumeona vile wameongeza betri kivyao kesho wataamka watwambie bei ya pikipiki sio 184,000 watwambie ni elfu 250.

Aidha wahudumu hao walisema kampuni ya Spiro imekiuka mkataba walioafikiana na wahudumu hao bila kuwahusisha washikadau husika wa sekta hiyo ya wanabodaboda.

 

Ile tulielewana hata wiki iliyopita tulipoenda pale showroom, tuliongea tukaelewana washukishe hii bei na tukamuomba hadi ile wakati tutaelewana akasema watabadili, lakini tumeona sasa iko pale pale juu,” alisema mhudumu mwengine.

Hata hivyo, meneja wa mauzo katika kampuni ya Spiro, Raymond Robert alisema wamechukua hatua hiyo ili kuzuia kampuni kukadiria hasara zaidi akisema bei ya awali waliyoafikiana na wahudumu hao ingebadilika kwa muda.

 

Wale stakeholders wengine pia tuliwaeleza sababu tulitoa taarifa hizi kwa sehemu zaidi ya tano, kuanzia pale stesheni zetu hadi katika mitandao ya kijamii tulitoa barua official. Tulipeana zaidi ya siku 5 kuhusu mabadiliko haya,” alisema.

Kadhalika meneja huyo amewataka wahudumu wa bodaboda kukumbatia mabadiliko hayo ya bei na ada hizo ili kukuza sekta hiyo ya uchukuzi kwa pamoja.

 

Tukiendelea na ile bei ya awali tulioweka pale mwanzo ni ya kujitambulisha kwa muda wote mrefu itakuwa ni hasara. Na haina haja tufanye biashara ya hasara,” alisisitiza Bw. Raymond.

Itakumbukwa kuwa ni miezi miwili tu tangu Rais William Ruto kuzindua Pikipiki zinazotumia umeme Kaunti ya Mombasa, uzinduzi alioutaja kuwa njia mojawapo ya kuimarisha sekta ya uchukuzi kwa kupunguza uchafuzi wa mazingira, kukabiliana gharama ya mafuta na ajali za barabarani.

BY NEWSDESK