HabariNewsUncategorized

Haki Yetu! Mabaharia Pwani Watishia Kuifikisha KMA Mahakamani

Muungano wa mabaharia Pwani umetishia kupelekea malalamishi yao bungeni iwapo mamlaka ya ubaharia nchini KMA haitaangazia haki zao za kikatiba.

Akizungumza na Sauti ya Pwani Naibu mwenyekiti wa Seafares Union of Kenya Albert Adembesa alisema mamlaka hiyo imekuwa ikikiuka haki ya mabaharia kwa upande wa ajira akidai kuwa baadhi ya wafanyikazi kwenye mamlaka hiyo hupokea hongo na kuajiri watu wengine mbali na walio na vigezo hitajika.

Aidha Adembesa alisema hatua hiyo itaweza kushinikiza bunge kutekeleza mikataba ya mabaharia huku akiongeza kuwa sheria ambazo zimewekwa zimetungwa kinyume na haki zao za kikatiba.

Sisi kama mabaharia tunataka zile haki zetu ambazo ziko kwa katiba,tupewe manake sheria zozote wanazotunga kinyume cha katiba na mkataba hatutazikubali na karibuni tutaandika mapendekezo na tutashinikiza bunge itekeleze, na tumejuwa watu kadhaa kwenye idara ya ubaharia wanakula milungula.’’ Alisema Adembesa

Adembesa aliongeza kuwa serikali imetengea wavuvi zaidi ya bilioni 2 huku ikiwatema wafanyibiashara wa kusafirisha mizigo kwenye meli licha ya wao kuwa na haki sawia akisistiza haja ya kusimama kupigana na ufisadi uliokithiri kwenye sekta hiyo.

Adembesa aliwaomba mawakala wa kuajiri kuhakikisha wanafanya matangazo ya nafasi za ajira wazi wazi kupitia vyombo va habari na magazeti.

Kila mawakala wa ajira watangaze kazi zao kwa njia ya radio,gazeti na Television ili kila mkenya aweze kuiona na aweze kutuma maombi, hatutakubali tena watu kupitia kwa kujuana kuendesha shughuli ya kuajiri.” Alisema Adembesa

Kwa upande wake Hassan Kombo mmoja wa mabaharia aliwataka viongozi waliochaguliwa kwenye sekta ya ubaharia kutoingiza siasa kwenye vyama mbali mbali akisema huenda hali hiyo ikaleta mgawanyiko miongoni mwao.

Nataka kuambia wale viongozi waliochaguliwa na rais Ruto aliwachagua kwa kazi za mamlaka ya ubaharia waache kuingilia mambo ya mabaharia, mambo ya kisiasa na kichama yetu waachane nayo waangalie kazi waliyopewa na Rais na mambo ya baharia kusomeshwa sisi tutajipanga na pia wasitugawanye.” Alisema Kombo

BY MEDZA MDOE