Rais William Ruto amebaini kuwa sasa bei ya mafuta itaendelea kushuka polepole katika siku zijazo.
Akizungumza huko kaunti Kisii katika Misa ya shukrani iliyoandaliwa katika Shule ya Upili ya Kadinali Otunga Mosocho rais alisema kuwa kushuka kwa bei ya mafuta ni ishara kuwa mikakati nah atua mwafaka zilizochukuliwa na serikali yake.
“Najua mambo ya mafuta imekuwa na shida lakini mnaona bei imeanza kushuka… sisi tutaendelea hivo,” alisema.
Alisisitiza kuwa licha ya bei za mafuta kuwa huaathiriwa sana na masuala ya Kimataifa, Kushuka kwa bei hizo sasa kumeashiria kuimarishwa kwa bei hizo duniani.
Rais alisisitiza kuwa Serikali yake imejitolea vilivyo kushusha gharama ya maisha huku akiwataka Wakenya kuwa na subira kwani serikali imeweka mipango kabambe ya kuimarisha zaidi Uchumi.
“Najua mmenipigia makofi lakini sii mimi napunguza au kuongeza bei …kuna majamaa wengine huko ng’ambo wao ndio wanatupea bei ya mafuta kila mwezi,” aliongeza.
Kiongozi huyo wa taifa aidha alisema Serikali imetumia mkakati wa kina katika kupunguza gharama ya maisha.
Rais alisema Serikali inasaidia wakulima ili kuongeza uzalishaji wa chakula, hatua aliyobaini kuwa inapunguza bei ya chakula.
“Mwaka jana, wakati kama huu mambo yalikuwa tofauti, bei ya unga ilikuwa shilingi 240 leo ni shilingi 140,” alisema.
Alisema Serikali pia inaongeza fursa kwa wananchi ili kuhakikisha wanapata mapato stahiki ili kujikimu.
Rais Ruto pia alisema matumizi ya Serikali yatapunguzwa na rasilimali za umma kutumika kwa busara kuwapa Wakenya thamani ya fedha zao.