HabariNewsUncategorized

Acheni Propaganda! Serikali ina pesa za kusimamia shughuli zake: asema Mwanaisha Chidzuga

Serikali inazo fedha za kutosha, haijafilisika na ina fedha za kuendesha shughuli zake kikamilifu.

Ni kauli yake Naibu Msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga akipuuzilia mbali madai kuwa serikali haina fedha za kutosha.

Akizungumza katika kipindi spedheli cha Gumzo na Sauti ya Pwani FM mnamo Jumamosi, Bi. Chidzuga alikariri kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto za kiuchumi serikali imejitahidi vilivyo kusimama imara.

Serikali haikosi fedha, haijafilisika na ina fedha za kutosha. Ingekuwa serikali haina pesa kama wanavyodai ulisikia wafanyakazi wa serikali amekosa mshahara…ulisikia wahudumu wa afya wale 1000 walikosa mshahara, hata walimu wameajiriwa,” alisema.

Alisema kuwa serikali imejikakamua vilivyo kutekeleza miradi yake mbali mbali licha ya kupata taifa katika hali ngumu ya kiuchumi.

Tumelipa madeni yetu hujasikia tumekosa kulipa, hapa Pwani bandari za uvuvi zinajengwa, Barabara zinajengwa, vipi serikali ikose fedha na tumetoa mbolea, tumeshukisha bei ya unga? Vipi serikali ikose fedha na hata tupunguza bei ya mafuta?” Alisema.

Wakati uo huo Chidzuga aliwataka viongozi mbali mbali wa kisiasa kukoma kueneza propaganda kuhusu serikali na badala yake kuunga mkono juhudi za serikali.

Amesisitiza kuwa mwelekeo wa Uchumi wa taifa upo katika hali nzuri akiahidi kuwa Serikali ya Kenya kwanza itazidi kuimarisha Uchumi kuhakikisha gharama ya maisha inazidi kushuka hata zaidi.

Hali iko shwari na itakuwa bora zaidi. Mafuta kupungua bei, kila kitu Uchumi kusonga hapa Kenya inategema mafuta, hivyo tukishukisha mafuta bei ya bidhaa mbalimbali zitashuka ni suala la muda tu, kwa hivyo tusipende kupinga kila kitu hiyo kasumba sisi kama Wakenya lazima tutoe katika akili kama kuna jema linafanyika pia tuseme,” alisema.

BY MJOMBA RASHID