HabariLifestyleNews

Mikakati kabambe yawekwa kuimarisha Utalii katika kaunti 4 za Pwani

Serikali imepania kuboresha sekta ya utalii ukanda wa Pwani kwa kufanya mageuzi mbalimbali pamoja kuboresha miundomsingi eneo hilo ili kuvutia watalii zaidi.

Akizungumza baada ya kikao na Magavana wa kaunti 4 za Pwani hapa Mombasa mnamo siku ya Jumatano, Waziri wa Utalii Alfred Mutua alieleza baadhi ya mikakati wanayopania kutekeleza katika jitihada ya kuboresha sekta ya utalii eneo la Pwani.

Mutua aliahidi kushirikiana na viongozi wa pwani kuboresha miundomsingi katika kaunti hizo ikiwemo kujenga vyoo na maduka ya jumla katika fukwe za bahari pamoja na kuimarisha usalama wa watalii wanaozuru maeneo hayo miongoni mwa mengine.

“Utalii pwani ni jambo muhimu sana tunapata fedha nyingi lakini tunaendesha suala hilo kwa asilimia 10. Sisi kama serikali kuu tunataka upande huu wa Pwani iwe ndio eneo la starehe na furaha katika Afrika.Tunataka kuboresha miundomsingi ,serikali kuu itatoa pesa ikishirikiana na magavana tujenge miundo ,tuinue utalii kwa njia ambayo inafaa.” Alisema Waziri Mutua.

Aidha Waziri huyo alidokeza kuwa serikali inapania kuunda kamati mbalimbali zitakazokabidhiwa majukumu ya kufanikisha utekelezwaji wa mipango ya kuboresha sekta ya utalii nchini.

Alibaini pia Serikali inapania kuanzisha mafunzo kwa wanajamii kuhusu jinsi ya kuishi na wanyamapori ili kupunguza mizozo ya kati ya wanyama hao na binadamu na kupunguza athari zinazotokana na suala hilo.

“Tuko na kamati nne, ya kwanza ikijumuisha magavana na mimi, halafu tuko na kamati ya uongozi wa utekelezaji,kutakuwa na timu ya kiufundi ya maafisa wakuu na wakurugenzi, kutakuwa na kamati za nyanjani kufuatilia jinsi kazi inavyoendeshwa,watu wote wanaohusika watakuwa kwenye kamati hizo.

Rais wetu amefungua taifa kwa ulimwengu wote, watu watajaa hapa lakini hatutaki watu wajae hapa low quality, low quality does not attract!” Alisisitiza Mutua.

Kwa upande wao magavana wa Pwani wameeleza matumaini yao kuwa Serikali itatua changamoto zinazokumba sekta hiyo ikiwemo ucheleweshwaji wa watalii wanaotumia kivuko cha Likoni-Ferry kuelekea Kwale pamoja na kuimarisha miundo ya angatua za ndege hapa pwani ili kufikia viwango vya kimataifa miongoni mwa changamoto nyinginezo.

“nina imani kwamba utalii ndani ya Kwale utazidi kunawiri, tunajua ikifika wakati wa festive season watalii wanapata shida ferry na tumekubaliana na waziri kuwa ataendelea kutusaidia.” Alisema Gavana Achani.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharif Nasser alisisitiza suala la kuwepo kwa mfumo wa anga huru ‘open-sky policy’ akiitaka serikali kuruhusu ndege za kimataifa kutua moja kwa moja katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Moi mjini Mombasa ili kupiga jeki sekta ya Utalii.

“Tunazidi kuiomba serikali iweze kufikiria tena mambo ya open skies, haya mambo yote tunayoyafanya yatakuwa hayana faida yoyote ikiwa watalii wenyewe watakuwa na shida ya kuweza kuingia Kenya.” Alisema Gavana Nassir.

 

Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro alibaini kuwa kando na kujitolea kuweka miundomsingi mwafaka, alisisitiza kuwa suala la mgogoro baina ya binadamu na wanyamaopori ni suala linalofaa kushughulikiwa na serikali kuu, ili utalii usiwe kikwazo kwa wakazi.

“Tutachangia pamoja kueka miundomsingi, tabu kubwa kilifi ni tatizo la wanyamapori ambayo tunapakana na mbuga ya wanyama ya Tsavo.” Alisema Gavana Mung’aro.

Issa Abdallah Timami ambaye ni Gavana wa Lamu naye alieleza kufurahishwa na ushirkiaono huo wa serikali Kuu na zile za kaunti katika kuwekeza kuimarisha utalii kanda hii ya Pwani.

“Tunafurahia vile waziri ametaka kufanya kazi pamoja na sisi na amejitolea kuwa serikali kuu itawekeza katika sekta ya utalii.” Alisema Gavana Timamy.

Mkutano huo umehudhuriwa na gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir, gavana wa Kwale Fatuma Achani, gavana wa Kilifi Gideon Mng’aro na gavana wa Lamu Issa Timamy pamoja na Mawaziri wa utalii kutoka kaunti hizo miongoni mwa wengine viongozi wengine.

BY BEBI SHEMAWIA