HabariNewsSiasa

Ni Hujuma! Rais Abatilishe kauli yake dhidi ya Mahakama; La sivyo…

Wanasheria nchini wametangaza kuandaa maandamano makubwa ya amani kote nchini juma lijalo ili kupinga na kukemea vikali hatua ya rais William Ruto kuishambulia idara ya mahakama.

Kupitia chama chao cha wanasheria nchini LSK, wanasheria wataandamana pia kushtumu hatua ya rais kuapa kukiuka maagizo ya mahakama ambayo amedai yanakwamisha miradi ya serikali yake.

Akihutubia wanahabari Jumatano, Rais wa LSK, Erick Theuri alisema mawakili wote na wanasheria watavaa riboni za rangi ya zambarau wakati wa maandamano hayo ili kuashiria kuunga mkono kwao mahakama na utawala wa sheria.

“Wanasheria wote watavaa riboni za njano na zambarau kuanzia wiki ijayo kuashiria uungaji mkono wao kwa utawala wa sheria. Tutakuwa na maandamano ya amani kote nchini kusimama na uhuru wa Mahakama. Tutaandamana kwa amani kuwasilisha ombi kwa Mwanasheria Mkuu.”

Mkuu huyo wa LSK ambaye alikuwa amendamana na viongozi wengine akiwemo naibu wake Faith Odhiambo alimtaka rais Ruto kubatilisha matamshi yake aliyotoa dhidi ya mahakama kwani anaweka historia mbaya ya utawala wa sheria nchini.

Wakati uo huo Theuri amemshinikiza rais Ruto kutoa ushahidi kwa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) dhidi ya maafisa fisadi ili hatua zichukuliwe kuliko kutoa madai yasiyo na uthibitisho wowote.

“Tunamtaka Rais wa Kenya atoe ushahidi wa ufisadi kwa JSC. Fisi akitaka kuwala watoto wake, huanza kwa kuwaambia kuwa wananukia kama kondoo,” alisema.

Alibainisha kuwa mashambulizi dhidi ya Idara ya Mahakama kwa matamshi kama hayo kutoka kwa kiongozi wa taifa pasi kufuata mfumo wa sheria uliowekwa ni ishara ya uongozi wa kiimla.

“Ikiwa Rais anasema hawezi kutii amri za mahakama, kipi kitatokea kwa mama mboga akisaka haki kortini?” Aliongeza.

BY MJOMBA RASHID