HabariNewsSiasa

Odinga amkemea Ruto kwa kuishambulia Korti; Aitaka Mahakama iwe imara

Idara ya Mahakama imetakiwa kusimama imara katika utendakazi wake na kupuuzilia mbali vitisho na matamshi ya Kiongozi wa Taifa dhidi yake.

Katika kikao na wanahabari mjini Mombasa kinara wa Azimio Raila Odinga aliwataka Majaji na mahakimu kutotishwa na shutma kutoka kwa rais Ruto kwa kuhakikisha wanaendeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba.

Raila amemkashifu rais Ruto kwa kutaka kurudisha uongozi wa kiimla kwa kuiteka mahakama kama alivyofanya kwa bunge la kitaifa.

Odinga aidha alisema maafisa wakuu serikalini wanaongoza kwa ufisadi kinyume na rais anavyotangaza kwamba mahakimu na majaji wanapokea hongo kuhujumu mipango yake.

Kiongozi huyo wa Azimio alisema kamwe hawataruhusu idara ya Mahakama kuingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake nchini.

Kauli yake inajiri baada ya rais William Ruto kudai kuwa Idara ya Mahakama inashirikiana na Wapinzani wa serikali kuididimiza mipango ya maendeleo Serikali iliyoiweka kwa ajili ya kumfaidi mwananchi.

BY BEBI SHEMAWIA